Skip to main content

Baraza la Usalama lakutana kuhusu vikwazo Somalia na Eritrea

Baraza la Usalama lakutana kuhusu vikwazo Somalia na Eritrea

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana leo kuhusu vikwazo vilivyowekewa Somalia na Eritrea, katika jitihada za kusaka amani kwenye eneo la Pembe ya Afrika.

Mwakilishi wa Kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa, ambaye pia ni rais wa Baraza la Usalama na mwenyekiti wa Kamati ya Vikwazo dhidi ya Somalia na Eritrea, Balozi Rafael Darío Ramírez Carreño, amesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kamati hiyo imepokea ripoti mbili, moja ikisema kuwa kuna hamu kubwa katika rasilmali za bahari na mali ghafi ya Somalia kutoka nchi za kigeni, ingawa hamu hiyo haijaenda sanjari na hatua mwafaka za kudhibiti rasilmali hizo.

Kuhusu sekta ya rasilmali za madini ya Somalia, kundi linaloripoti limesema kunaongezeka utata kati ya serikali kuu ya Somalia na mamlaka za mikoa, kwani zote zinaendelea kutia saini mikataba na mashirika ya kimataifa ya mafuta na gesi.”

Kuhusu tishio la Al Shabaab kwa Somalia na Pembe ya Afrika, amesema

“Kundi hilo limeripoti kuwa bado tishio hilo lipo. Al Shabaab imetumia udhaifu wa idadi ndogo ya vikosi vya AMISOM, jeshi la kitaifa na vikosi vya pamoja, na kwa hiyo ngome za vikosi hivi zinaendelea kuwa hatarini kushambuliwa.”