Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliokosa misaada kwa kipindi kirefu Syria wafikiwa leo asubuhi - WFP

Waliokosa misaada kwa kipindi kirefu Syria wafikiwa leo asubuhi - WFP

Baada ya zaidi ya mwaka mmoja na nusu bila misaada yoyote ya kibinadamu huku wakikumbwa na mashambulizi, hatimaye wakazi wa miji mitano huko Syria leo wameweza kupata misaada muhimu ya kibinadamu.Flora Nducha na taarifa kamili

(Taarifa ya Flora)

Mkurugenzi mkazi wa WFP Syria Jakob Kern amesema hatua ya leo ni ya kipekee kwa wakazi wa miji ya Moadamiyeh, Zabadani na Madaya iliyoko Damascus vijijini na ile ya Foah na Kefraya iliyoko Idlib vijijini.

Amesema shehena za misaada zimepakuliwa usiku na asubuhi ya leo kutoka magari ya mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Isam Ismail ni afisa wa WFP ambaye amekuwepo wakati wa upakuaji wa shehena hizo.

(Sauti ya Isam)

“Huu ni msafara wa kwanza kabisa tangu mwezi Julai  mwaka 2014 na sasa WFP inawapatia mgao wa familia wa chakula kwa raia wote Elfu 45 waliosalia hapa. Watu wengi ni wakimbizi wa ndani na inatia huruma kuona mazingira wanaomishi. Hata wale wanaoishi hapo wako kwenye majengo ambayo yameharibiwa.”

WFP imetaka pande kinzani kwenye mzozo huo kuzingatia umuhimu wa wananchi kupata misaada ikisema ni matumaini yao wataweza kuendelea kupeleka misaada kwani mahitaji ni ya kila siku ikiwemo vyakula, maji na dawa.

WFP nchini Syria inaendelea kuwapatia chakula zaidi ya watu Milioni Nne kila mwezi na bado inasalia na wasiwasi kuhusu machungu wanayopata wananchi walio kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikika.