Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa chakula washika kasi Sudan Kusini- FAO

Uhaba wa chakula washika kasi Sudan Kusini- FAO

Sudan Kusini inakabiliwa na kiwango cha kisicho cha kawaida cha ukosefu wa chakula ambapo karibu asilimia 25 ya wananchi wake wanahitaji msaada wa dharura wa chakula. Joseph Msami na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Joseph)

Kaimu mwakilishi wa FAO nchini humo Serge Tissot amesema shirika hilo na lile la mpango wa chakula duniani WFP wanatiwa shaka na idadi hiyo kwani inaongezeka wakati huu ambao ni msimu baada ya mavuno, kipindi ambacho kwa kawaida huwa wana chakula cha kutosha.

Idadi inatarajiwa kuongezeka zaidi msimu wa mwambo ambao ni kati ya mwezi Aprili na Julai na hivyo wadau wa kibinadamu wametoa ripoti wakisema kipindi hicho kitakuwa kirefu zaidi kuliko miaka ya awali.

Mashirika hayo yametaka kutekelezwa haraka kwa mkataba wa amani ili kuwezesha biashara kurejea sambamba na watoa misaada waruhusiwe kufika maeneo yote kuwasilisha misaada kule inakohitajika zaidi.