Skip to main content

WHO yahaha kutafiti mwenendo wa virusi vya Zika

WHO yahaha kutafiti mwenendo wa virusi vya Zika

Shirika la afya duniani, WHO limesema linahaha kuandaa miradi ya utafiti na kusaidia tafiti nyingine ili kupata uelewa zaidi jinsi virusi vya Zika vinavyoenezwa, katika mazingira yapi na kwa njia zipi nyingine zaidi ya ile ya sasa kupitia mbu aina ya Aedes.

Msemaji wa WHO Gregory Hartl amesema hayo Geneva, Uswisi leo kufuatia shuku na shaka juu ya njia nyinginezo ambazo kwazo virusi hivyo vinaweza kuenezwa.

(Sauti ya Hartl)

“Kwa sasa hatuna majibu ya maswali haya. Tunachofahamu sasa karibu asilimia 100 ya wagonjwa wanatokana na maambukizi kupitia mbu. Kwa hiyo kwa WHO, jambo la msingi kufanya sasa ni kuhakikisha watu hawang’atwi na mbu.”

Amesema robo tatu ya watu wanaoambukizwa virusi hivyo hawaonyeshi dalili zozote, ilhali robo iliyobakia wanakuwa na dalili ndogo kama vile homa, upele na mafua, dalili ambazo amesema hupotea ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja.

Bwana Hartl amesisitiza hatua za kujikinga kwa  kuondoa madimbwi ambayo ni mazali ya mbu na kupuliza dawa pamoja na kupakaa dawa za kujikinga na mbu.