Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 32 zimekumbwa na virusi Zika, Ulaya yahadharishwa ijikinge – WHO

Nchi 32 zimekumbwa na virusi Zika, Ulaya yahadharishwa ijikinge – WHO

Shirika la afya duniani WHO limesema idadi ya nchi ambazo zimeripoti uwepo wa virusi vya Zika imefikia 32 nchi hizo zikiwemo Afrika, Amerika, Kusini-Mashariki mwa Asia na Pasifiki Magharibi. Priscilla Lecomte na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Priscilla)

Barani Afrika ni nchi moja tu Cabo Verde imeripoti kirusi hicho ambapo Waziri wake wa afya Dokta Cristine Fontes Lima amesema…

(Sauti ya Cristine)

“Ni Kweli napenda kutuma ujumbe wa kujiamini kuwa hapa Cabo Verde tumeweza kudhibiti mgonjwa huyo na sasa tuna maambukizi ya virusi hivyo vya Zika na sasa tuko kwenye mwelekeo wa kupunguza mlipuko wake.”

Huko Ulaya licha ya kwamba hakuna iliyoripoti tayari Mkurugenzi wa WHO kwenye ukanda huo Dkt. Zsuzsanna Jakab amezitaka nchi za Ulaya kuwa makini na kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya virusi vya Zika wakati huu misimu ya chipukizi na joto ikikaribia.

Dkt. Jakab amesema kila nchi barani Ulaya ambako mbu aina ya Aedes anayeeneza virusi hivyo anapatikana, iko hatarini kwa kuwa idadi ya wasafiri walioambukizwa Zika wameingia, lakini ugonjwa haujabainika kwa kuwa vijidudu bado vimepoa.

Hatua za kujikinga ni pamoja an kudhibiti mazalia ya mbua, kupuliza dawa ya kuua mbu, kuelimisha umma hususan wanawake wajawazito na kuchagiza tafiti kuhusu Zika ili kupata mbinu za kubaini na chanjo.