Kumbukizi ya Holocaust, Ban atoa ujumbe jamii iache kubagua
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga na manusura wa mauaji ya halaiki ya Holocaust, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kumbukizi hii inadhihirisha kile kinachoweza kutokea iwapo binadamu atasahau utu wao.
Katika ujumbe wake Ban amesema mauaji ya Holocaust dhidi ya wayahudi yalikuwa uhalifu mkubwa ambao hadi sasa hakuna mtu anayeweza kupinga kuwa yalitokea na hivyo kumbukizi yake ni hatua ya kurejelea azma ya kuzuia vitendo hivyo visitokee tena.
Amesema kwa mantiki hiyo kila mtu anapaswa kukataa na kutupilia mbali itikadi za kidini na kisiasa ambazo zinajenga chuki na kubagua watu.
Badala yake ametaka watu kuachana na chuki dhidi ya wayahudi na mashambulizi kwa misingi ya imani ya dini, kabila na makundi mengine akisema kuwa nivyema kujenga dunia yenye utangamano na kuheshimiana na ambamo kwayo amani ni ya kudumu.