Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo kuhusu Syria yasogezwa hadi Ijumaa: de Mistura

Mazungumzo kuhusu Syria yasogezwa hadi Ijumaa: de Mistura

Mazungumzo kuhusu Syria yaliyokuwa yaanze leo, Geneva, Uswisi, yamesogezwa mbele hadi Ijumaa wiki hii ya tarehe 29.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura ametangaza hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva akisema yatafanyika kwa miezi Sita.

Amesema mialiko kwa washiriki inatarajiwa kuanza kusambazwa Jumanne na kwamba majadiliano kuhusu washiriki wa mazungumzo hayo baina ya wasyria bado yanaendelea.

(Sauti ya de Mistura)

“Mialiko itatolewa kwa kuzingatia vigezo vya ujumuishi na hali halisi iliyopo. Ajenda itakuwa ile iliyowekwa na azimio namba 2254. Mialiko kwa dhahiri itawalenga pia wanawake na mashirika yasiyo ya kiraia, nimeweka wazi, halikadhalika Katibu mkuu amekuwa wazi kuhusu hilo, orodha au waalikwa wowote watakaotaka kushiriki,  tutahakikisha kuna ushiriki wa kutosha wa wanawake kwa ajili ya kunishauri ili tuhakikishe tuko  katika mwelekeo sahihi kuhusu hatma ya Syria ambako wao ni karibu asilimia 51."

Awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo itakuwa ya wiki mbili au tatu ikijikita katika masuala ya usitishaji mapigano, kudhibiti kikundi cha ISIS na kuongeza misada ya kibinadamu.