Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yahimiza utulivu kufuatia hali tete Darfur Magharibi

UNAMID yahimiza utulivu kufuatia hali tete Darfur Magharibi

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika Darfur, UNAMID, umeeleza kutiwa hofu na hali tete inayoendelea katika mji wa El Geneina na karibu na kijiji cha Mouli, yapata kilomita 15 kutoka El Geneina, Darfur Magharibi. Kwa mantiki hiyo, UNAMID imetoa kwa mamlaka za serikali kufanya juhudi zote kuidhibiti hali.

Taarifa ya UNAMID imesema kuwa hali hiyo tete imeibuka kufuatia kikundi kisichojulikana kukivamia kijiji cha Mouli mnamo Januari 9 2016, na kusababisha idadi kubwa ya wanakijiji hicho kukimbilia El Geneina.

Raia hao waliofurushwa makwao walifanya maandamano mjini El Geneina mnamo Januari 10, na kusababisha kufungwa kwa shule na biashara mjini humo.

UNAMID imekuwa ikipokea ripoti za kuendelea machafuko na ufyatuaji risasi wa mara kwa mara kote El Geneina na Mouli, na idadi isiyojulikana ya wahanga wa machafuko hayo.

Ujumbe huo umetoa wito kwa pande zote katika mzozo kujidhibiti, huku ukiahidi kusaidiana na mamlaka za jimbo ili kutuliza hali kwa njia ya amani.