Mchakato wa amani Mali bado ni dhaifu: Baraza la Usalama

Mchakato wa amani Mali bado ni dhaifu: Baraza la Usalama

Leo Baraza la Usalama limejadili hali ya usalama na kibinadamu nchini Mali pamoja na kufuatilia operesheni za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA.

Akihutubia kikao hicho, mkuu wa idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani, Hervé Ladsous amesisitiza umuhimu wa kutekeleza maazimio ya makubaliano ya amani, akisema utekelezaji wake ukizidi kuchelewa, hasa kwa upande wa utaratibu wa kusalimisha vikundi vilivyojihami, huenda mapigano yataanza upya.

Bwana Ladsous ametumia hotuba hiyo kupongeza jitihada za serikali ya Mali, pande kinzani za mzozo na jamii ya kimataifa katika kuhakikisha kwamba mapigano yamesitishwa.

Hata hivyo amesema bado juhudi na mabadiliko yanahitajika katika maswala ya kusalimisha askari, kuandaa uchaguzi wa serikali za mitaa na kuleta mabadiliko katika mfumo wa kisiasa kaskazini mwa nchi.

Aidha amemulika tishio la ugaidi akieleza kwamba asilimia 94 ya askari zaidi ya 11,000 wanaotumikia MINUSMA nchini Mali wanashughulikia usalama wa MINUSMA yenyewe, akiongeza..

(Sauti ya Bwana Ladsous)

"Mchakato wa amani unaoanza nchini Mali bado ni dhaifu na unakumbwa na changamoto kubwa. Miezi iliyopita imeonyesha utashi wa vikundi vya kigaidi kuharibu mchakato wa amani. Mizizi ya mzozo ni wa kisiasa, na nasisitiza kwamba hakutakuwa na suluhu ya kisiasa bila mabadiliko ya kisiasa na kitaasisi yaliyoamuliwa na makubaliano ya amani."