Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 2 zahitajika kwa ajili ya Sahel 2016:UM

Dola bilioni 2 zahitajika kwa ajili ya Sahel 2016:UM

Mashirika ya Umoja wa mataifa na washirika wake leo wamezindua ombi la msaada wa kibinadamu kwa ajili ya Sahel kwa mwaka 2016. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Ombi hilo la kikanda linahitaji dola bilioni 1.98 ili kutoa msaada wa mahitaji muhimu ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu walioathirika na migogoro katika nchi 9 za Afrika ukanda wa sahel.

Kwa mujibu wa msaidizi wa Katibu Mkuu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu kanda ya Sahel Toby Lanzer mchanganyiko wa athari za mabadiliko ya tabianchi, umasikini uliokithiri, ongezeko la haraka la idadi ya watu, na kuongezeka kwa kasi kwa machafuko na kutokuwepo usalama kunaathiri maisha ya watu, mali zao na mustakhbali wa jamii ambazo zina hali mbaya kabisa duniani.

Amesema hivyo wanahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa ili kuhakikisha kwamba mamilioni ya watu wanaweza kupata hasa mahitaji ya lazima na ulinzi wanaostahili ili kuishi maisha yenye hadhi. Mwaka 2016 watu wapatao milioni 23.5 hawatakuwa na chakula cha kutosha huku wengine milioni 6 wakihitaji msaada wa dharura wa chakula.