Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon akariri umuhimu wa kuzuia mauaji ya kimbari

Ban Ki-moon akariri umuhimu wa kuzuia mauaji ya kimbari

Leo ikiwa ni mara ya kwanza ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya kukumbuka wahanga wa mauaji ya kimbari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni fursa ya kukariri umuhimu wa kuhakikishia mauaji kama hayo hayatokei tena na kuhakikishia wahanga wanapata matibabu na fidia jinsi inavyotambuliwa na sheria ya kimataifa.

Kwenye ujumbe wake Bwana Ban amesema ili kuzuia mauaji hayo ni lazima kufuatilia dalili za mapema na kujitahadhari ili kukabiliana nazo, akieleza kwamba mauaji ya kimbari hayatokei kama ajali, bali yanapangwa kwa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusu maadhimisho ya siku hii mshauri maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Adam Dieng amesema ni muhimu kukumbuka wahanga na kuzuia hali isitokee tena huku akigusia Burundi akisema..

(Sauti ya Dieng)

''Ni wakati wa kuchukua hatua. Natiwa hofu sana na matumizi ya ukabila toka pande zote, serikali na upinzani. Historia ya Burundi ni ya machafuko. Kwa kuzingatia kile kilichotokea Rwanda mwaka 1994 , hatuwezi kupuuza umuhimu wa kuchuka hatua mapema''