Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji ya kiafya ya wanawake baada ya majanga hupuuzwa:Ripoti

Mahitaji ya kiafya ya wanawake baada ya majanga hupuuzwa:Ripoti

Mahitaji ya kiafya ya wanawake na wasichana barubaru mara nyingi hupuuzwa wakati wa harakati za usaidizi wa kibinadamu zinazofanyika baada ya mizozo au majanga.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya hali ya idadi ya watu duniani iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA iliyopatiwa jina hifadhi baada ya janga.

Mathalani ripoti imesema kati ya watu Milioni 100 wanaohitaji misaada ya kibinadamu duniani kote, Milioni 26 ni wanawake na wasichana walio kwenye umri wa kuweza kupata watoto.

Na kama hiyo haitisho, kila siku wanawake 507 katika nchi zenye majanga na vita hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi na kujifungua.

Kwa mantiki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Babatunde Osotimehin amesema afya na haki za kundi hilo hazipaswi kuonekana ni jambo la baadaye wakati wa usaidizi wa kibinadamu.

Badal yake amesema kwa mjamzito ambaye anakaribia kujifungua au msichana barubaru ambaye ameepuka ukatili wa kingono, huduma za kuokoa maisha ni muhimu kama ilivyo maji, chakula na malazi.

Amesema bila huduma kama hiyo, kundi hilo liko hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa kingono, ujauzito usipangwa na hata maambukizi kama vile VVU.