Skip to main content

Upatikanaji wa ARV msingi wa kutokomeza ukimwi: bara la Afrika laongoza

Upatikanaji wa ARV msingi wa kutokomeza ukimwi: bara la Afrika laongoza

Wakati wa kuelekea siku ya kimataifa ya ukimwi tarehe mosi mwezi Disemba, Shirika la Afya Duniani WHO limesisitiza kwamba kueneza upatikanaji wa matibabu yanayopinga virusi hivyo (ARV) ni msingi wa kutokomeza mlipuko wa ukimwi kwa kipindi cha kizazi kimoja.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo, WHO imesema kwamba upatikanaji wa ARV umechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kwa asilimia 42 vifo vitokanavyo na ukimwi tangu mwaka 2004.

Tayari watu milioni 16 wanapata matibabu ya ARV miongoni mwa milioni 37 walioambukizwa na ukimwi, na wengi wao wako barani Afrika ambapo kwa mujibu wa WHO idadi kubwa zaidi ya watu wanaweza kupata matibabu hayo kuliko mabara mengine.

Ili kufikia lengo la kuongeza maradufu idadi ya watu wanaopata ARV ifikapo mwaka 2020, WHO imependekeza kuraisisha vipimo na upatikanaji wa matibabu.