Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani kutunguliwa kwa ndege ya Urusi mpakani na Syria

Ban alaani kutunguliwa kwa ndege ya Urusi mpakani na Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ana wasiwasi mkubwa na kitendo cha jeshi la Uturuki kutungua ndege ya kijeshi ya Urusi hii leo.

Hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wake Stephane Dujarric alipokuwa akijibu swali la waandishi wa habari mjini New York, Marekani akisema kuwa..

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu anasihi pande zote kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kuepusha kuendeleza zaidi mzozo huu. Ni matumaini yake kuwa tathmini ya kina na makini kuhusu tukio hili itatoa taswira sahihi na hivyo kusaidia lisitokee tena siku za baadaye.”

Bwana Dujarric amerejelea wito wa Katibu Mkuu wa kutaka wale wote wanaotumia anga kudhibiti magaidi kuhakikisha wanazingatia kanuni ikiwemo kulinda raia.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Novemba Balozi Matthew Rycroft  aliulizwa juu ya athari za kitendo hicho..

(Sauti ya Balozi Rycroft)

‘Kinatushinikiza kuongeza maradufu juhudi zetu. Ni lazima tusake suluhu la kisiasa kwenye mzozo wa Syria na wakati huo huo tuhakikishe kuna hatua sahihi zisizo na mkanganyiko ili kuepusha hali kama hii kutokea tena.”

Amesema yeye kama Rais wa Baraza anasubiri iwapo nchi yoyote itataka kuitishwa kwa kikao na wako tayari kufanya hivyo lakini hadi sasa hajapokea ombi lolote.