Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITU yafikiria kubadilisha mahesabu ya wakati

ITU yafikiria kubadilisha mahesabu ya wakati

Kongamano la Kimataifa kuhusu masafa ya radio lililoandaliwa na shirika la mawasiliano duniani, ITU linaendelea huko Geneva Uswisi ambapo limeamua kufuatilia uwezekano wa kubadilisha uratibu wa muda kimataifa unaoanzia Uingereza, UTC.

Lengo ni kuondoa sekunde inayoongezwa mara chache ili kurekebisha tofauti kwenye mzunguko wa sayari ya dunia na kubaki sambamba na wakati wa jua.

Sekunde hiyo inayosogezwa, iliongezwa mara ya mwisho tarehe 30, mwezi Juni mwaka huu dakika moja kabla ya saa sita za usiku.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo, ITU ambayo jukumu lake pia ni kutuma taarifa sahihi kuhusu wakati kote duniani hadi angani, imesema iwapo sekunde hiyo haitaongezwa tena, mifumo yote inayotumia teknolojia za kompyuta na saa, hasa mifumo ya kuongoza boti baharini, haitahitaji tena kubadilisha wakati wao, na hivyo itabaki sahihi daima.

ITU imesema dunia inazidi kutegemea mifumo inayohitaji kubaki sambamba na wakati, na kwa hiyo litashirikiana na wadau wote wa kimataifa ili kupata maamuzi thabiti kuhusu swala hilo.