Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rushwa, usafirishaji haramu wa fedha na mali zilizoibwa vyamulikwa

Rushwa, usafirishaji haramu wa fedha na mali zilizoibwa vyamulikwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Kudhibiti madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, Yury Fedotov, amepongeza kutambuliwa kwa rushwa na hongo kama suala la kuzingatiwa chini ya lengo namba 16 la maendeleo endelevu, SDGs, wakati wa mkutano wa sita wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa (COSP6), ambao unafanyika mjini St. Petersburg, Urusi.

Katika kikao kuhusu kupambana na rushwa na utekelezaji wa SDGs, Bwana Fedotov amesema ofisi yake inakaribisha kutambua kwa jamii ya kimataifa kuwa lengo namba 16 kuhusu kujenga taasisi zifaazo, zinazowajibika na jumuishi linahusu mambo mengi.

Ameongeza kwamba kupunguza rushwa na hongo, pamoja na kushughulikia usafirishaji haramu wa fedha na kuokoa mali zilizoibwa, ni muhimu katika kuendeleza ukuaji wa uchumi na uwekezaji.

Hatua kama hiyo inahitajika pia, iwapo tunataka kukabiliana na uhalifu wa kupangwa na ukatili, kukomesha unyanyasaji na usafirishaji haramu wa watoto na wanawake, kutunza mazingira, kuhakikisha uzalishaji na matumizi endelevu, kupunguza utofauti na kujenga miundo mbinu dhabiti.”

Akizungumza kwenye tukio hilo, Msaidizi wa Katibu Mkuu katika idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii, Wu Hongbo amesema mkutano huo unatoa fursa ya kuwa na mdahalo kuhusu kupinga rushwa na ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu.

Kupinga rushwa ni sehemu muhimu ya Ajenda 2030, siyo tu kwa sababu kumetajwa moja kwa moja katika lengo la SDG namba 16 na lengo dogo namba 5, lakini pia kwa sababu kunahusu juhudi zetu zote za kutimiza SDGs na malengo madogo husika.”