Ban azungumza na Kikwete kuhusu uchaguzi Zanzibar

Ban azungumza na Kikwete kuhusu uchaguzi Zanzibar

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambapo pamoja na kumpongeza kwa uchaguzi wa Tanzania amezungumzia pia suala la uchaguzi wa Zanzibar.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema Ban ameeleza wasiwasi wake kuhusu kile kinachoendelea Zanzibar akisisitiza kuwa mamlaka za uchaguzi zinapaswa kuonekana zinatekeleza majukumu yake kwa ueledi, bila upendeleo na kwa kasi kubwa.

Ametoa wito kwa Rais Kikwete kuhakikisha shaka zote zitokanazo na mchakato mzima wa uchaguzi huo wa Zanzibar zinashughulikiwa kwa taratibu za kisheria zilizopo.

Bwana Ban pia amemsihi Rais Kikwete atoe wito kwa wadau wote wasalie na utulivu na kuepuka matumizi yoyote ya ghasia au kutoa matamko yanayoweza kuongeza zaidi mvutano.