Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Tanzania: Ban apongeza wananchi, asalia na wasiwasi kuhusu Zanzibar

Uchaguzi Tanzania: Ban apongeza wananchi, asalia na wasiwasi kuhusu Zanzibar

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa taarifa ya kupongeza serikali ya Tanzania, vyama vya siasa na wananchi wake kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo tarehe 25 mwezi huu wa Oktoba, akisema umekuwa wa amani.Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ban amenukuliwa katika taarifa ya msemaji wake akisema kuwa kitendo cha wananchi wa Tanzania kuwajibika kwa kupiga kura na kusubiri matokeo ya uchaguzi ni ishara ya azma yao ya kuendeleza demokrasia amani na utulivu.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema anasalia na wasiwasi juu ya hali ya Zanzibar ambako uchaguzi na matokeo yake yamefutwa.

Ban amesisitiza umuhimu wa mzozo unaohusiana na mchakato wa uchaguzi ushughulikiwe kwa kuzingatia taratibu za kisheria na kwa uwazi.

Ametoa wito kwa wadau wote kuwa na utulivu na kujizuia kutumia ghasia na fujo, sambamba na kuepusha kutoa matamko ambayo yanaweza kuongeza mvutano.

Katika uchaguzi huo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM John Magufuli ameibuka mshindi kwa kupata zaidi ya asilimia 58 ya kura zote halali zilizopigwa.

Kufuatia kuchaguliwa kwake, Rais huyo mteule baada ya kuapishwa  atakuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa sheria.