Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM asema biashara ya kimataifa izingatie haki za binadamu

Mtaalam wa UM asema biashara ya kimataifa izingatie haki za binadamu

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji wa utaratibu wa kimataifa wa demokrasia na haki, Alfred de Zayas, amesema kuwa biashara ni lazima itumike kuendeleza haki za binadamu na maendeleo na siyo ya kudunisha haki.

Katika ripoti yake ya nne kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bwana de Zayas amemulika athari za mikataba ya biashara na uwekezaji huria dhidi ya haki za binadamu, na hivyo kutaka utaratibu  wa usuluhishi wa utata unaoambatana na kusainiwa mikataba hiyo baina ya serikali na wawekezaji (ISDS) ipigwe marufuku.

Amesema katika miaka 25 iliyopita, mikataba ya kimataifa na ile ya biashara huria inayojumuisha usuluhishi wa utata baina ya serikali na wawekezaji imeathiri vibaya utaratibu wa kimataifa na kanuni za msingi za Umoja wa Mataifa, uhuru wan chi, demokrasia na utawala wa sheria.

Ameongeza kuwa badala ya kuendeleza haki za binadamu, mikataba hiyo au ISDS imedhoofisha wajibu wa serikali wa udhibiti, na hivyo kuchangia kukosekana kwa usawa baina ya mataifa na ndani ya mataifa.