Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM kuzindua huduma ya simu kusaidia jamii nchini Burundi

IOM kuzindua huduma ya simu kusaidia jamii nchini Burundi

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM limezindua huduma mpya kupitia kwa simu ili kuwapatia watu wanaoishi Burundi taarifa mbali mbali kuhusu usaidizi wa kibinadamu. Joseph Msami na taarifa kamili,

(Taarifa ya Msami)

Taarifa iliyotolewa leo na IOM imesema kuwa mradi huo mpya umeundwa kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali na ya Umoja wa Mataifa, wakati ambapo machafuko nchini Burundi tayari yamesababisha watu 200,000 kuikimbia nchi na wengine wengi wakiwa wakimbizi wa ndani.

Kupitia nambari ya simu + 257 2227 4010, mtu yeyote anayeishi nchini Burundi anaweza kupata taarifa kuhusu misaada na huduma zinazopatikana, kuanzia jumatatu mpaka ijumaa, saa 12.30 asubuhi hadi saa 12.30 jioni.

Kristina Mejo ni Mkurugenzi wa IOM nchini Burundi.

(Sauti ya Kristina)

« Tunaweza kufikia hali ambapo uvumi unasambazwa haraka, kwa hiyo tunatarajia kuwapatia taarifa mara moja, sahihi na za kuaminika, ili watu waweze kuchukua uamuzi wakiwa wamefahamishwa kuhusu wasiwasi wao au kuhusu uamuzi ambao walikuwa wanatarajia kuchukua kwenye siku zijazo. »

Kadhalika mradi huo unalenga kukusanya taarifa za moja kwa moja kuhusu mahitaji ya jamii zilizoko nchini Burundi na kuimarisha uratibu wa misaada.