Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana 3 kati ya 10 katika nchi zenye zahma hawajasoma:UNICEF

Vijana 3 kati ya 10 katika nchi zenye zahma hawajasoma:UNICEF

[caption id="attachment_337036" align="alignleft" width="300"]dailynews023b-18

Vijana 3 kati ya 10 wa umri wa miaka 15 hadi 24, sawa na vijana milioni 59 wanaoshi katika nchi zilizoathirika na vita au majanga hawajasoma, hii ikiwa ni mara tatu ya kiwango cha kimataifa imesema ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo nchi za Niger, Chad, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR zenye historia ya kutokuwepo utulivu na kiwango cha juu ya umasikini ni maskani ya idadi kubwa ya vijana wasiojua kusoma wala kuandika, zikishikilia asilimia 76, 69, 68 na 64 wa umri huo.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta H. Fore amesema idadi hiyo ni kumbusho la athari kubwa zinazosababishwa na migogoro na majanga kwa elimu ya watoto, mustakhbali wao, utulivu, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii zao.

Ameongeza kuwa kijana anayekua katika hali ya kutojua kusoma wala kuandika, kwenye nchi iliyoghubikwa au kusambaratishwa na vita au majanga , huenda asiwe na fursa yoyote nzuri katika maisha yake.

Uchambuzi wa ripoti hii umetokana na viwango vya kutojua kusoma na kuandika vilivyowekwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO kwa nchi 27 zilizo katika hali ya dharura kote duniani kwa sababu ya zahma mbalimbali.

Ripoti pia inasema wasichana na wanawake ndio idadi kubwa ya wasiosoma ikiwa ni asilimia 33 ikilinganishwa na asilimia 24 ya wavulana.

Sasa UNICEF inahitaji takribani dola bilioni 1 kwa ajili ya programu zake za elimu kwa mwaka huu 2018.