Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha vijana wasio na ajira bado kiko juu: ILO

Kiwango cha vijana wasio na ajira bado kiko juu: ILO

Shirika la kazi duniani, ILO limesema zaidi ya vijana milioni 73 duniani kote hawana ajira, na idadi hiyo, inatarajiwa kuongezeka ikizingatiwa utofauti wa mazingira ya kuimarika kwa uchumi wa baadhi ya maeneo ya duniani.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya kila mwaka ya ILO inayoonyesha kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana bado uko kiwango cha juu kuliko kabla ya  mtikisiko wa uchumi duniani mwaka 2008.

Mataifa yaliyoathirika zaidi ni yale yaliyoko Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambapo karibu vijana watatu kati ya 10 hawana ajira.

Azita Berar Awad ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera ya Ajira ILO.

(SAUTI Azita Berar Awad)

"Hakuna shaka kuwa ukosefu wa  ajira hususan kwa vijana wa kike kwenye ukanda huo ni suala la kimuundo ambalo haliwezi kushughulikiwa kwa ukuaji uchumi pekee."