Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 tangu tetemeko la ardhi Pakistani, usalama shuleni waangaziwa

Miaka 10 tangu tetemeko la ardhi Pakistani, usalama shuleni waangaziwa

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza hatari ya majanga, UNISDR, Margareta Wahlström amesema shule inapaswa kuwa eneo salama zaidi baada ya nyumbani.

Ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni miaka 10 tangu tetemeko kubwa la ardhi lipige Pakistani na kuuwa watu elfu 87 ambao kati yao Elfu 19 walikuwa watoto wa shule na walimu.

Watoto na walimu hao walikuwa shuleni tetemeko lenye ukubwa wa nyusi 7.8 katika kipimo cha richa lilipopiga majira ya saa Mbili na dakika 50 asubuhi muda mfupi tu baada ya masomo kuanza.

Bi. Wahlstrom amesema katika maeneo yaliyo ukanda wa matetemeko ya ardhi na ambako misingi ya ujenzi haizingatiwi shule zinaweza kugeuka makaburi ya watoto na walimu.

Kwa mantiki hiyo Mkuu huyo ambaye anaongoza mkutano wa nchi 25 kuhusu shule salama, amesema mpango huo wa shule salama unaweza kutoa utaalamu kwa nchi zilizo kwenye ukanda huo kuimarisha au kubomoa shule zilizo hatarini zaidi.

Tayari Iran na Uturuki zimenza kuzingatia misingi ya shule salama na ametoa wito kwa nchi nyingie kujiunga.