Mjumbe wa UM Yemen akaribisha hatua ya wahouthi
Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed amekaribisha taarifa ya hivi karibuni zaidi ya kikundi cha wahouthi nchini humo ya kukubali azimio nambari 2216 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameeleza kuwa katika taarifa yao, wahouthi wamesisitiza azma yao ya kuzingatia misingi saba ya makubaliano ya Muscat yaliyowasilishwa na kikundi hicho.
Bwana Dujarric amemnukuu mjumbe huyo akisema kuwa hiyo ni hatua muhimu kwani azimio namba 2216 la baraza la usalama na mengineyo, mpango wa ushirikiano wa nchi za ghuba, GCCI na matokeo ya mashauriano ya kimataifa yamekuwa ni kitovu cha mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kwa hiyo..
(Sauti ya Dujarric)
“Mambo haya makuu matatu yatasalia kuwa misingi ya mazungumzo ya amani ambayo mjumbe huyo amekuwa akishughulikia. Bwana Ahmed anaamini kuwa serikali ya Yemen, wahouthi na washirika wao watakubali mwaliko kujiunga katika mazungumzo kwa misingi hii.”