Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wazindua kanuni za Nelson Mandela kuhusu haki za wafungwa

UM wazindua kanuni za Nelson Mandela kuhusu haki za wafungwa

Leo kwenye Umoja wa Mataifa zimezinduliwa kanuni za Nelson Mandela kuhusu wafungwa, ambazo zinaweka viwango wastani vya chini zaidi vya kushughulikia haki na maslahi ya wafungwa.

Akikaribisha kanuni hizo, rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft, amesema..

(Sauti ya Lykketoft)

“Wafungwa ni wanadamu, waliozaliwa kwa utu, na wanastahili kuwa salama na haki zao kulindwa. Kanuni za Mandela zinathibitisha kuwa wafungwa wote wanapaswa kuheshimiwa, na kwamba wafungwa wote watalindwa kutokana na utesaji, na vitendo na adhabu zingine za kikatili au zinazowadhalilisha”

Miongoni mwa marekebisho yaliyofanyiwa kanuni hizo za viwango wastani vya kushughulikia maslahi ya wafungwa ni kuhakikisha kuwa wafungwa wanafurahia haki ya kuwa na afya sawa na watu wengine, kuhakikisha hakuna mtu anayetengwa na watu kizuizini kwa zaidi ya saa 22 mfululizo.

Pia zinatoa mwongozo mpya wa uchunguzi wa vifo, kutoweka au majeraha mabaya kwa wafungwa, na kuwaruhusu wafungwa kupata huduma za wakili wa sheria.