Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa inakiuka sheria ya kimataifa- wataalam wa UM

Adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa inakiuka sheria ya kimataifa- wataalam wa UM

Serikali zimekumbushwa leo kuwa mauaji ya watu wanaokabiliwa na makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa. Hayo ni kwa mujibu wa wataalam maalum wa Umoja wa Mataifa, wakiwa ni anayehusika na mauaji ya kiholela, Christof Heyns na mtaalam kuhusu utesaji, Juan E. Méndez.

Inakadiriwa kuwa hukumu zinazohusu dawa za kulevya huenda zikawa zinachangia mauaji ya watu wapatao 1,000 kila mwaka kote duniani.

Wakizungumza kabla ya maadhimisho ya 13 ya Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani, ambayo ni Oktoba 10, wataalam hao wamesema kutolewa hukumu za kifo na mauaji kwa makosa ya dawa kunaongeza kwa kiwango kikubwa idadi ya watu duniani wanaojikuta katika adhabu hiyo ambayo ni kinyume na kanuni za msingi za haki za binadamu.

Aidha, wamesema zaidi ya nchi 30 zina sheria zinazoruhuru adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya, na kwamba katika baadhi ya nchi, zikiwemo Indonesia, Uchina, Iran na Ufalme wa Saudia, visa hivyo huchangia kiwango kikubwa cha idadi ya mauaji.