Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gharama ya kupuuza mahitaji makubwa ya kibinadamu eneo la Ziwa Chad, itakuwa kubwa- O’Brien

Gharama ya kupuuza mahitaji makubwa ya kibinadamu eneo la Ziwa Chad, itakuwa kubwa- O’Brien

Mratibu Mkuu wa masauala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Stephen O’Brien, ameonya leo kuwa jamii ya kimataifa ikipuuza mahitaji makubwa ya kibinadamu katika eneo la Ziwa Chad, gharama yake itakuwa kubwa zaidi.

Bwana O’Brien amesema hayo katika mkutano wa ngazi ya juu kujadili mzozo wa kibinadamu unaoibuka katika eneo hilo, na kuona njia bora za kuwasaidia mamilioni ya watu ambao usalama wao umo hatarini, sambamba na wanavyotegemea kusihi.

Mkuu huyo wa OCHA amesema kuwepo mizozo mingi ya kimataifa kumefanya taabu inayowakabili watu wa eneo la Ziwa Chad kutomulikwa, licha ya kuwa moja ya mahali penye watu wengi zaidi kulazimika kuhama makwao, kwani watu wapatao milioni 2.3 wamelazimika kuhama makwao tangu mwezi Mei 2013.

“Ingawa wengi wao wapo Nigeria, Boko Haram wamesababisha maafa makubwa, kwa kushambulia kiholela vijiji, wakiwaua wanaume na kuwateka wanawake na watoto katika nchi zote nne. Watu katika eneo la Ziwa Chad ni miongoni mwa watu masikini zaidi na thabiti zaidi duniani, na sasa ukanda huo umekuwa pia uwanja wa ghasia na hofu.”

Aidha, Bwana O’Brien ametaja aina nyingine za taabu wanazokumbana nazo watu wa eneo hilo

“Ukame na mafuriko hulikumba eneo hilo mara kwa mara. Utapiamlo na milipuko ya magonjwa vimetanda kwa viwango vya dharura. Watu wapatao milioni 5.5 hawana chakula cha kutosha, au hawawezi kupata chakula chenye lishe. Kipindupindu ni tishio la mara kwa mara, vikiwa vimeripotiwa visa 37,000 na vifo 760 Cameroon, Niger na Nigeria mwaka jana.”

Ametaja pia tishio la Boko Haram, na jinsi linavyowaathiri wanawake na watoto, ambao wanatekwa, kubakwa na kusafirishwa kiharamu, wakilazimishwa kufanya kazi kama wachukuzi, na watoto wadogo kutumiwa katika mashambulizi ya kujitoa mhanga.