Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Francis kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo

Papa Francis kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo

Leo ikiwa ni siku ya kwanza ya mkutano wa kuridhia malengo ya maendeleo endelevu au SDGs ambao unajumuisha viongozi wa dunia mjini New York Marekani kwa siku tatu, Mkuu wa kanisa la katoliki Papa Francis anatarajiwa kutembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za kimataifa katika kutokomeza umaskini na kuleta ustawi wa jamii.

Akiwa makao makuu wakati wa mkutano , Papa Francis atatoa hotuba mbele ya Baraza kuu ambapo Mwakilishi wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, Roger J. Landry ameiambia Redio ya Umoja wa Mataifa kuwa hii ni mara ya tano kiongozi wa kanisa katoliki anahutubia baraza kuu ingawa kwa Papa Francis ni mara ya kwanza.

Landry ameeleza kwamba Papa Francis anatarajiwa kushukuru Umoja wa Mataifa kwa jitihada zake katika kutekeleza malengo ya masharti yake ambayo baadhi yao yanaenda sambamba na maadili ya kanisa katoliki ikiwemo kupambana na majanga ya vita, kutunza haki za binadamu, na kukuza maendeleo.

« Anajali sana mahitaji ya watu maskini. Kwa hiyo nadhani tutasikia mengi kuhusu watu maskini, atakuwa sauti ya nchi 47 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambako watu ni mafukara wa kutupwa wakiishi kwa kutumia chini ya dola moja na senti 25 za kimarekani kwa siku. »

Hatimaye amesema anatarajia kuwa Papa Francis atazingatia umuhimu kwa nchi wanachama kuheshimu makubaliano yao ya kimataifa, kwani kutimiza ahadi ni moja ya maadili ya wakristo duniani kote.