Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutimiza SDGs kutahitaji kubadilisha njia za uzalishaji na matumizi ya chakula- FAO

Kutimiza SDGs kutahitaji kubadilisha njia za uzalishaji na matumizi ya chakula- FAO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, Jose Graziano da Silva, amesema leo kuwa kilimo na maendeleo ya vijijini vinapaswa kupewa msukumo mkubwa ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya kutokomeza umaskini na kutokomeza njaa, ambayo yamepitishwa leo.

Akiongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanafanya changamoto za kutimiza malengo hayo kuwa kanganyifu zaidi, Bwana da Silva amesema kutimiza malengo hayo kutahitaji mabadiliko makubwa katika njia za uzalishaji na matumizi ya chakula.

Mkuu huyo wa FAO amekuwa akizungumza mjini New York katika mjadala kuhusu umaskini na njaa, kama sehemu ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu.

Akitaja kupitishwa kwa malengo 17 ya maendeleo endelevu kama uamuzi wa kihistoria, Bwana da Silva amesema inawezekana kutokomeza umaskini na njaa katika kizazi hiki, lakini akaongeza kuwa hilo litahitaji mabadiliko haraka, yakiwemo kufanya mifumo ya kilimo na chakula kuwa yenye kuzalisha zaidi, jumuishi zaidi na thabiti zaidi, huku ikiwa na uzalishaji mdogo zaidi wa gesi chafuzi.