Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wathiriwa pakubwa na vita nchini Yemen, UNICEF

Watoto wathiriwa pakubwa na vita nchini Yemen, UNICEF

Vifaa muhimu vya maji  vilivyonuiwa kuwasaidia watu 11,000 katika maeneo yaliyoathiriwa pakubwa na vita nchini Yemen vimeharibiwa jana baada ya ghala linalotumiwa na shirika la kibinadamu katika mji wa Dhamar kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sana'a kuharibiwa katika shambulizi la bomu.

Katika taarifa, Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen, Jeremy Hopkins amesema, UNICEF imesikitishwa na uharibifu wa vifaa hivyo vya kibinadamu, ambavyo ni pamoja na mitungi ya maji, vifaa vya kusafisha maji na matenki ya maji.

Aidha, Hopkins amesema mashambulizi hayo yanawaathiri raia na haiwezi kukubaliwa.

Halikadhalika, Hopkins amesema nchini Yemen, tangu mwezi Machi mwaka huu, angalau watoto 466 wameuawa na wengine 658 kujeruhiwa kufuatia mapigano makali.

Baada ya kuchacha kwa vita mwezi Machi 2015, UNICEF imeweza kuthibitisha shule 41 na hospitali 61 zimeshambuliwa au kuharibiwa kwa sababu ya mapigano.