Skip to main content

Tumepiga hatua za ubia kwa maendeleo, lakini bado kuna mianya- Ban

Tumepiga hatua za ubia kwa maendeleo, lakini bado kuna mianya- Ban

Ripoti mpya iliyozinduliwa leo kuhusu lengo namba nane la maendeleo ya milenia, imeonyesha kuwa, licha ya ufanisi uliopatikana katika kufikia malengo kadhaa, bado kuna mianya mikubwa katika kupunguza hatari zinazozikumba nchi maskini, nchi zisizo na pwani na nchi za visiwa vidogo zinazoendelea.

Ripoti hiyo iitwayo, “Tathmini ya Ubia wa Kimataifa kwa Maendeleo,” imeandaliwa na kikosi kazi alichoweka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2007, kwa minajili ya kufuatilia hatua za kutimiza lengo namba nane la maendeleo ya milenia, ambalo linahusu ubia wa kimataifa kwa maendeleo.

Akiizindua ripoti hiyo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema ripoti ya mwaka huu ina umuhimu wa aina yake, ikiwa imekuja wakati nchi wanachama zinapojiandaa kupitisha na kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030.

“Ripoti ya kikosi kazi kuhusu mianya katika MDG imebaini pia njia za kuboresha ubia wa kimataifa kwa maendeleo miaka ijayo, hususan kupitia ufuatiliaji ulioimarishwa zaidi, na uratibu bora zaidi wa aina nyingi za ubia zinazoongezeka. Mpito kutoka kwa MDGs kwenda SDGs unatoa fursa ya kufungua rasilmali za uwekezaji katika elimu, afya, ukuaji ulio sawa, na uzalishaji na matumizi endelevu.”

Ban ametoa wito kwa wadau duniani waitikie msukumo unatokana na fungu jipya la malengo kabambe ya maendeleo endelevu.