Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda unayoyoma kwa Ulaya kutatua mzozo wa wakimbizi: UNHCR

Muda unayoyoma kwa Ulaya kutatua mzozo wa wakimbizi: UNHCR

Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR limesema muda unayoyoma kwa bara la Ulaya kushughulikia sakata la wakimbizi na wahamiaji na kwamba hali iliyopo sasa inaweza kutumbukiza wasaka hifadhi hao kwenye mikono ya wasafirishaji haramu. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amebainisha kuwa kauli yao inazingatia zahma iliyoshuhudiwa jana kwenye mpaka kati ya Serbia na Croatia na kwamba hali itazidi kuwa mbaya kutokana na kuendelea kuwasili kila siku kwa wakimbizi wapya.

Amesema wanaunga mkono hatua ya bunge la Ulaya kuunga mkono mpango wa kuwahamishia  wakimbizi Laki moja na elfu Ishirini kwenye nchi nyingine za Ulaya na kwamba ..

(Sauti ya Adrian)

Kikao kisicho cha kawaida cha tarehe 22 Septemba cha baraza la haki na mambo ya ndani na kile cha baraza la Ulaya cha tarehe 23 mwezi huu vitakuwa muhimu kwa maafikiano. Vikao hivi vinaweza kuwa ni fursa za mwisho kwa suluhu chanya na ya pamoja ya Ulaya katika kushughulikia janga hili.”

Mwaka huu pekee wakimbizi na wahamiaji zaidi ya Laki Nne wamewasili Ulaya kupitia bahari ya Mediteranea ambapo zaidi ya 2,900 wamefariki dunia na UNHCR inasema wimbi hilo linaongezeka kila uchao na wanahamishwa kutoka nchi moja kwenye nyingine bila suluhu la kudumu la hifadhi.