Skip to main content

UNICEF yalaani vikali mashambulizi dhidi ya watoto Mjini Allepo, Syria

UNICEF yalaani vikali mashambulizi dhidi ya watoto Mjini Allepo, Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limelaani vikali mashambulizi ya makombora yaliyofanyika jana katika maeno ya raia mjini Aleppo ambapo angalau watoto 19 waliuawa ikiwa ni pamoja watoto sita waliokuwa katika eneo salama linalofadhiliwa na shirika la UNICEF.

Katika taarifa, UNICEF imesema shambulizi hili la kukemewa linaonyesha kwamba hata kitendo rahisi cha kucheza ni hatari kubwa kwa watoto nchini Syria, na kuongezea kuwa katika wiki za karibuni, mashambulizi kadhaa ya kiholela yameripotiwa katika maeneo wanakoishi raia na kusababisha vifo na majeruhi  kwa watoto kadhaa.

Aidha, Shirika hilo limesema mashambulizi haya yanaonyesha uvunjaji hadharani wa sheria za vita na hatua hiyo ni dhihirisho tosha kuwa hakuna eneo salama kwa watoto nchini Syria.

Kwa maantiki hiyo, UNICEF imetoa wito kwa pande zote husika katika mgogoro wa Syria kusitisha mara moja mashambulizi hayo na kuchukua hatua za kuwalinda raia na maeneo kama vile shule, vituo vya afya na vituo vya maji, kwa mujibu wa sheria ya kibinadamu ya kimataifa, kwani, raia wote wakiwemo watoto ni  lazima walindwe wakati wowote.