Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya NANSEN yaenda kwa mkimbizi wa Afghanistan

Tuzo ya NANSEN yaenda kwa mkimbizi wa Afghanistan

Mwalimu mkimbizi kutoka Afghanistan, Aqeela Asifi ameshinda tuzo yam waka huu ya wakimbizi ya NANSEN.

Tuzo hiyo inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR imezingatia jinsi Bi. Asifi alivyojitolea maisha yake kuwapatia elimu watoto wakimbizi wa kike wa Afghanistan walioko nchini Pakistani.

Taarifa ya UNHCR imesema imetambua ujasiri wake anapofanya kazi hiyo kwenye kijiji cha wakimbizi cha Kot Chandana huko Mianwali Pakistan wakati akihaha kukimu maisha yake ugenini.

Mathalani imesema licha ya rasilimali ndogo na changamoto za kitamaduni, Asifi amewaongoza maelfu ya watoto wa kike wakimbizi kuhitimu elimu yao ya msingi.

Afghanistan inaongoza kwa raia wake wengi kuishi ukimbizini ambapo takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya raia wake Milioni Mbili na Nusu wanaishi nje ya nchi  yao na nusu yao ni watoto.