Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tatizo la wakimbizi Ulaya lahitaji juhudi za pamoja- Guterres

Tatizo la wakimbizi Ulaya lahitaji juhudi za pamoja- Guterres

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema leo kuwa hali ya wakimbizi Ulaya inahitaji juhudi kubwa za pamoja, ambazo haziwezekani kupatikana kwa kufuata mtazamo wa sasa uliogawanyika. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Bwana Guterres amesema hayo wakati Muungano wa Ulaya ukiandaa mikutano ya dharura katika jitihada za kushughulikia mzozo ulioko sasa wa wakimbizi na wahamiaji.

Amesema wale ambao wanathibitika hawahitaji hifadhi ya kimataifa na hawawezi kunufaika na fursa za uhamiaji halali wanapaswa kusaidiwa kurejea makwao haraka kwa kuzingatia haki zao za kibinadamu. Melissa Flemming ni msemaji wa UNHCR Geneva.

(sauti ya Melissa)

"Ulaya inahitaji kuchukua hatua sahihi, hakuna nchi moja inaweza kufanya hivyo peke yake, hakuna nchi moja au mbili, au tano miongoni mwa nchi 28 inaweza kupokea idadi kubwa ya watu wanaotafuta hifadhi, kila nchi inahitajika kutekeleza jukumu lake, na nchi ambazo hazina uwezo wa kushughulikia kiwango hiki kikubwa cha wahamiaji, zinastahili kusaidiwa haraka na kwa kiwango kikubwa sana."

Ulaya inakabiliwa na mmiminiko mkubwa zaidi wa wakimbizi katika miongo kadhaa, watu 300,000 wakiwa wameyaweka maisha yao hatarini kuvuka Bahari ya Mediterenia mwaka huu pekee.

Zaidi ya watu 2,600 wamefariki dunia wakijaribu kuvuka bahari hiyo, akiwemo mtoto aitwaye Aylan mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye picha yake imeibua mwamko mkubwa katika mioyo ya watu kote duniani.