Skip to main content

UNSOM yalaani shambulizi la Al Shabaab huko Somalia

UNSOM yalaani shambulizi la Al Shabaab huko Somalia

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay, amelaani vikali shambulio la leo kwenye kituo cha kikosi cha ujumbe wa Afrika nchini Somalia, AMISOM huko Janaale, mkoa wa Shabelle chini.

Shambulio hilo katika kituo hicho kinachosimamiwa na walinda amani kutoka Uganda limesababisha vifo ambapo Bwana Kay ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Uganda na Somalia.

Mwakilishi huyo ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOM amenukuliwa akisema walinda amani waliopoteza maisha ni jasiri na walijitoa mhanga maisha yao ili kuleta amani  na usalama wa kudumu nchini humo.

Amesema Umoja wa Mataifa licha ya shambulio hilo la Al Shabaab, umejizatiti kusimama kidete na wananchi wa Somalia na kusisitiza kuwa mshikamano wao na AMISOM na vikosi vya usalama vya Somalia katika kutokomeza Al Shabaab hautatetereshwa.