Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tunataka kuhudumia watu Taiz:WHO

Chonde chonde tunataka kuhudumia watu Taiz:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetaka kuwepo kwa maeneo salama ya kutoa huduma za afya ili liweze kudhibiti kuenea kwa homa ya Denge au kidinga popo kwenye jimbo la Taiz nchini Yemen wakati huu ambapo mashambulizi yanaendelea dhidi ya vituo vya afya na wagonjwa kushindwa kupata huduma.

Mkurugenzi wa WHO kwa kanda ya Mashariki na Mediteranea Dkt. Ala Alwani amesema ombi lao linazingatia kasi ya ongezeko la visa shukiwa vya ugonjwa huo ambapo mwanzoni mwa mwezi huu vilikuwa 145 lakini vimeongezeka hadi 421 tarehe 25 mwezi huu.

Amesema wana hofu kuwa hali inaweza kuwa mbaya kutokana na kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama na watu zaidi ya Milioni Tatu wanashindwa kupata huduma za afya huko Taiz.

Pamoja na ombi hilo WHO imetangaza hatua za kuchukua kudhibiti Kidinga popo ambazo ni kupuliza dawa kwenye majengo ili kuua mbu wanaoeneza Kidingapopo, kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo, kusambaza vyandarua vilivyoweka viuatilifu na kuimarisha usimamizi kwa kufuatilia wagonjwa na kuimarisha maabara.