Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya ukosefu wa maji Syria inatisha : UNICEF

Hali ya ukosefu wa maji Syria inatisha : UNICEF

Huku kukiwa na ukatili usioisha nchini Syria,  majira ya joto kali ni miongoni mwa ushahidi kuwa pande kinzani nchini humo zinatumia maji kufanikisha malengo yao kijeshi na kisiasa.

Taarifa zinasema kuwa katika miezi ya hivi karibuni takribani watu milioni tano wanaoishi mijini na jamii nchini humo zimeteseka tena wakati mwingine kwa makusudi kwa kukosa maji.

UNICEF imetoa ripoti kuwa mjini Aleppo ambapo mapigano yameathiri vituo vya mifereji kwa miezi sasa, zaidi ya mara 18 maji yamekatwa kwa makusudi . Shirika hilo linasema kuwa baadhi ya jamii zimeachwa hadi siku 17 mfululizo bila maji huku wengine hadi mwezi mzima.

Mkuu wa UNICEF ukanda wa Masharaiki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika Dk Peter Salama amesema maji safi ni haki ya msingi na hitaji la lazima nchini Syria kama ilivyo popote pale. Ukosefu wa maji umesababisha bidhaa hiyo kupanda bei kwa asilimia 3000 ya kawadia nchini humo.