Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha makubaliano kuhusu mazungumzo kwenye rasi ya Korea

Ban akaribisha makubaliano kuhusu mazungumzo kwenye rasi ya Korea

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha kwa moyo mkunjufu makubaliano yaliyofikiwa leo baina ya Jamhuri ya Korea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK.

Katibu Mkuu amesema amefurahia hasa makubaliano ya kufanya mazungumzo mara kwa mara baina ya nchi hizo mbili, na kwamba hiyo itakuwa njia mwafaka ya kudhibiti matatizo yoyote yatakayoibuka kwenye rasi ya Korea.

Aidha, Ban ameunga mkono kwa dhati hatua za kibinadamu, kama vile kukutanisha familia zilizotenganishwa bila kuzingatia masuala ya kisiasa na kiusalama.

Bwana Ban pia amesema anatarajia kuwa msukumo huo mpya uliopatikana kwa mazungumzo baina ya nchi hizo mbili utachangia kuanzisha tena mazungumzo ya kushughulikia suala la nyuklia.

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kutekeleza makubaliano hayo kikamilifu kwa amani na ustawi wa rasi ya Korea.