Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 6,000 wakimbilia kituo cha UNMISS Malakal kuepuka njaa

Zaidi ya watu 6,000 wakimbilia kituo cha UNMISS Malakal kuepuka njaa

Idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 6,000 wamelazimika kuhama makwao katika wilaya ya Wau Chollo nchini Sudan Kusini, na kukimbilia kituo cha ulinzi wa raia cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS kutokana na njaa ilozuka katika eneo hilo.

Watu wanaowasili wanasema kuna uhaba wa chakula, huduma za afya na mahitaji mengine ya kibinadamu, wakitoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu yawape usaidizi katika kituo cha UNMISS.

Kaimu mratibu wa UNMISS katika jimbo la Upper Nile, Isiaka Adesola Abolurin, amesema UNMISS na wadau wa kibinadamu wanashirikiana kutoa usaidizi kwa watu hao wanaowasili upya, ingawa wanakumbana na upungufu wa vifaa vya misaada kutokana na vikwazo vya serikali na changamoto za kiusafiri.

“Jukumu la UNMISS na mamlaka yake ni kuwalinda raia. Tunatakiwa kutoa ulinzi na kuhakikisha kuna usalama kwa wote walioko ndani ya vituo vya ulinzi wa raia na nje yake. Tunatakiwa pia kutoa nafasi ya wahudumu wa kibinadamu kujenga mahema. Kuhusu chakula, maji na huduma za afya, hilo ni jukumu la wadau wa kibinadamu. Lakini UNMISS inahakikisha kuwa chakula kinapotolewa, tunatoa ulinzi ili kisipiganiwe.”