Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapokumbuka Hiroshima, tuchukue hatua kutokomeza silaha za nyuklia- Ban

Tunapokumbuka Hiroshima, tuchukue hatua kutokomeza silaha za nyuklia- Ban

Ikiwa leo ni miaka 70 tangu shambulio la bomu kwenye mji wa Hiroshima nchini Japan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema maadhimisho ya siku hii yanapaswa kuwa ukumbusho kwa watu wote duniani, kwamba kuna haja ya kuchukua hatua ya dharura kutokomeza kabisa silaha za nyuklia.

Katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Bwana Kim Won-soo, ambaye ni Kaimu Mwakilishi Mkuu kuhusu masuala ya uondoaji silaha, Katibu Mkuu amesema miongo saba baada ya matumizi ya kwanza ya silaha za nyuklia katika mzozo, maadhimisho hayo ya huzuni ni ya kuwakumbuka makumi ya maelfu ya watu waliofariki dunia siku hiyo, na kuwaenzi manusura ambao wamekabiliwa na maafa makubwa tangu wakati huo.

Bwana Ban ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unashikamana nao katika ari ya kutaka kutimiza ndoto ya ulimwengu usio na silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu amesema wakati huu Umoja wa Mataifa unapoadhimisha pia miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, jamii ya kimataifa ni lazima iendeleze juhudi zake hadi pale silaha za nyuklia zitakapotokomezwa.