Ban na Obama wajadili masuala mseto Washington

4 Agosti 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa amekuwa na mazungumzo mazuri na muhimu na Rais Barack Obama wa Marekani leo, kabla ya mkutano wa kihistoria wa Baraza Kuu mwezi Septemba, na pia baada ya rais huyo kupiga hatua kadhaa za ufanisi kidiplomasia, zikiwemo kuafikia mkataba wa nyuklia na Iran, kurejesha uhusiano na Cuba na ziara yake ya kihistoria Afrika.

Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi habari mjini Washington Marekani, ambako pia amepongeza mpango Rais Obama alioutangaza hapo jana wa nishati huishi isiyochafua mazingira, akiutaja kama wenye kufungua fursa za ajira na kulinda sayari dunia kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Katibu Mkuu amesema wamejadili kuhusu jinsi ya kuchagiza dola bilioni 100 kufadhili tabianchi, akisema hilo ni muhimu hususan sasa, baada ya ufanisi walifikia kwa kuafikia ajenda ya maendeleo endelevu, yenye malengo 17, pamoja na kuafikiwa mkakati wa ufadhili wa maendeleo mjini Addis Ababa mwezi uliopita.

Kuhusu Syria, Bwana Ban amesema watajaribu kuongeza kasi ya kutekeleza andiko la Geneva, huku wakijitahidi kutoa usaidizi wa kibinadamu kwa wahitaji.

Kuhusu Yemen, Ban amesema hali nchini humo inawasikitisha, akiongeza kuwa hakuna suluhu la kijeshi kwa mzozo nchini humo uliowaacha zaidi ya watu milioni 21 wakihitaji usaidizi wa kibinadamu. Amesema suluhu kwa mzozo huo ni la kisiasa tu, kupitia mazungumzo.

Aidha, amemsifu Rais Obama pia kuhusu Sudan Kusini, kufuatia mkutano wake na viongozi wa Afrika, ambao umeibua matumaini ya kusainiwa makubaliano ya kuumaliza mzozo nchini humo mnamo Agosti 17.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter