Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mauaji ya Jenerali Nshimirimana wa Burundi

Ban alaani mauaji ya Jenerali Nshimirimana wa Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na kuendelea kuzorota kwa mazingira ya usalama nchini Burundi kufuatia kipindi cha uchaguzi kilichoghubikwa na machafuko na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi.

Katika muktadha huo, Ban amelaani vikali kuuawa kwa Jenerali Adolphe Nshimirimana hapo jana Agosti 2, na kukaribisha ujumbe wa Rais Nkurunziza kwa taifa wa wito wa kudumisha utulivu, na kwa mamlaka husika kuchunguza haraka mauaji hayo na kuwafikisha washukiwa mbele ya sheria.

Akiwahutubia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu ametoa wito kwa mamlaka za Burundi kuchunguza mauaji mengine kwa misingi ya kisiasa.

Katibu Mkuu amekariri wito wake kwa Warundi wote warejelee mazungumzo jumuishi bila kukawia, na kutatua tofauti zao kwa njia ya amani, chini ya uongozi wa Rais Museveni kama ilivyoamrishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katibu Mkuu ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha amani na kuzuia mzozo nchini Burundi.”