Sitisho la mapigano Yemen ni muhimu sasa kuliko wakati wowote:O’Brien

8 Julai 2015

Wakati mamilioni ya wananchi wa Yemen wakiendelea kuhaha kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao, Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amesema sitisho al mapigano ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati wowote ili kufikisha mahitaji kwa raia.

Taarifa ya ofisi yake ambayo inaratibu misaada hiyo, OCHA imemnukuu akisema kuwa pande katika mzozo huo ni vyema zikubali kusitisha mapigano bila masharti yoyote kwani mashambulio ya sasa yasiyochagua maeneo yametumbukiza raia kwenye njaa.

Amesema mashambulizi hayo yameharibu miundombinu ya kijamii ikiwemo hospitali, shule na hata masoko kwa hiyo wananchi wanakosa huduma za msingi wakati huu abmapo asilimia 80 ya wananchi wote wa Yemen wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Bwana O’Brien amesema pande katika mzozo huo lazima zizingatie sheria za kibinadamu za kimataifa ambazo zinasisitiza ulinzi wa raia na maeneo yao wakati wa mizozo.

Ameitaka pia jamii ya kimataifa kutumia ushawishi wake ili kuhakikisha wakiukaji wa haki za binadamu nchini Yemen wanawajibishwa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter