Bara la Afrika limefanikiwa zaidi katika kutimiza MDGs: ripoti
Bara la Afrika limetimiza mafanikio makubwa zaidi kuliko maeneo mengine duniani katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia MDGs, hasa kuhusu maswala ya afya na elimu.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo kuhusu utekelezaji wa MDGs tangu 1990.
Ripoti imesema Afrika iliyoko chini ya jangwa la Sahara imefanikiwa kuongeza kiwango cha uandikishwaji shuleni kutoka asilimia 52 mwaka 1990 hadi asilimia 80 mwaka 2015. Halikadhalia, usawa wa kijinsia umeimarika, hadi bungeni, ambapo nchi 4 kati ya 10 zinazoongoza duniani kwa uwiano wa wanawake bungeni ziko barani Afrika, huku Rwanda ikiwa ya kwanza na asilimia 60 ya wabunge wakiwa ni wanawake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kutoka Norway, rais wa Rwanda Paul Kagame amesema panapo utashi wa kisiasa, mafanikio yanapatikana.
“ Tumeona kwamba mshikamano wa viongozi na wananchi unahitajika ili kutimiza malengo. Tunajua matokeo ni bora wakati ambapo nchi zinawajibika kuhusu ajenda yao ya maendeleo ndani ya ushirikiano wa kimataifa wenye heshima.”
Aidha ripoti imeonyesha mafanikio katika kupunguza idadi ya maambukizi mapya ya ukimwi, ambayo yamepungua kwa asilimia 50, na idadi ya vifo vitokanavyo na malaria, vilivyopungua kwa asilimia 49.
Hata hivyo, bado changamoto zipo, ripoti ikionyesha kwamba bado asilimia 40 ya watu waliopo barani Afrika wanaishi chini ya kiwango cha umaskini.