Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti inayotathmini ufanisi wa MDGs yazinduliwa

Ripoti inayotathmini ufanisi wa MDGs yazinduliwa

Ripoti ya tathmini ya mwisho ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia, MDGs. imezinduliwa leo, ikionyesha mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini duniani kote. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na Idara ya Maswala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa DESA, idadi ya watu wanaoishi kwenye hali mbaya zaidi ya umaskini imepungua kwa nusu, kutoka bilioni 1.9 mwaka 1990 hadi milioni 836 mwaka 2015.

Aidha mafanikio yamepatikana kwenye maeneo mengine, yakiwemo usawa wa kijinsia, afya ya watoto na wanawake wajawazito, pamoja na kupambana na ukimwi na malaria.

Hata hivyo ripoti imeonyesha tofauti kubwa baina ya maeneo na nchi, huku watu wengine wakiachwa nyuma kimaendeleo. Akizindua ripoti hiyo kutoka Norway Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, akiwa pamoja na waziri mkuu wa Norway Erna Solberg na rais wa Rwanda Paul Kagame,  amezingatia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa:

“ Mafanikio yetu yanaonyesha kuwa hatua za pamoja zina ufanisi. Hapa kwenye Umoja wa Mataifa, tumeonyesha kwamba kushirikisha wadau muhimu, serikali, jamii, sekta binafsi na watafiti, kunaharakisha mafanikio. Tunapaswa kushirikiana ili kumaliza kazi iliyoanza na MDGs na kujenga juu ya mafanikio hayo na msukumo huo.”