Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya CAR bado yashindwa kulinda raia mikoani : Mtalaam wa UM

Serikali ya CAR bado yashindwa kulinda raia mikoani : Mtalaam wa UM

Mtalaam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Keita Bocoum, ametaka serikali nchini humo kuimarisha uthabiti wake mikoani ili iweze kulinda raia dhidi ya mashambulizi. Taarifa zaidi na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Katika taarifa aliyotoa leo baada ya ziara yake ya siku saba nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR awali mwezi huu, Bi Keita amesema wawakilishi wa serikali ni wachache sana mikoani. Ametolea mfano alipotembelea maeneo ya Boali ambako amesema hakuna mahakama na mkuu wa polisi ana wasaidizi wanne pekee akisema hawatoshi kuhakikisha usalama wa raia.

Ametaja baadhi ya changamoto zinazokumba CAR kuwa ni ukwepaji sheria kwa watekelezaji wa uhalifu dhidi ya haki za binadamu, mashambulizi dhidi ya raia na uhalifu dhidi ya watoto, hasa wale ambao ni wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo mtalaam huyo amewapongeza raia wa CAR kwa hatua walizochukua katika kuelekea amani na maridhiano, akitaja mafanikio ya Kongamano la Bangui na ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza bidii ili kuisaidia nchi hii kufanikiwa katika wakati huu wa mpito.