Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaiomba EU kuchukua hatua zaidi kusaidia wakimbizi

UNHCR yaiomba EU kuchukua hatua zaidi kusaidia wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema leo kwamba uamuzi wa Muungano wa Ulaya wa kusajili wasaka hifadhi 40,000 pamoja na kuwapa makazi wakimbizi 20,000 ni hatua muhimu katika kutatua mzozo huu wa uhamiaji lakini bado hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa, ikiwemo kukabiliana na misingi ya mzozo huo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amesema ni muhimu Muungano wa Ulaya uonyeshe uongozi na dira katika kukabiliana na changamoto hii, wakati huu ambapo watu wanazidi kuwasili Italia na Ugiriki.

“ Wakati Baraza la Ulaya linatambua umuhimu wa kushirikiana na nchi za asili na nchi za kupitia, sababu za msingi zinapaswa kukabiliwa. Juu ya hayo, sasa operesheni kubwa za kibinadamu kama Syria na Jamhuri ya Afrika ya Kati hazina ufadhili wa kutosha. Kupitia usaidizi uliolengwa zaidi, ikiwemo miradi ya maendeleo, uwezo wa wakimbizi wa ndani wa kujitegemea utaimarishwa.”

Aidha UNHCR imeziomba nchini wanachama wa Muungano wa Ulaya kuwapa wahamiaji njia mbadala za kuhamia kihalali barani Ulaya, na kuwezesha familia kuungana kwa ufanisi zaidi, ikisema hayo yatasaidia kupunguza usafirishaji haramu wa wahamiaji.