Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yabadili mwelekeo wa usaidizi NEPAL, ukata ukibisha hodi

WFP yabadili mwelekeo wa usaidizi NEPAL, ukata ukibisha hodi

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limebadili mwelekeo wake wa usaidizi nchini Nepal kwa lengo la kutoa misaada huku likisaidia harakati za nchi hiyo kujikwamua baada ya matetemeko ya ardhi ambayo yalisababisha vifo pamoja na uharibifu wa miundombinu. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mratibu wa masula ya dharura wa WFP nchini humo Richard Ragan amesema mwelekeo sasa ni wapagazi ambao sambamba na kupandisha milimani misaada ya vyakula na vifaa vya ujenzi wa kliniki za muda, wanarekebisha njia za milimani ambazo zilikuwa hazipitiki baada ya matetemeko ya ardhi, kazi ambayo wanafanya kwa ujira.

Amesema ni kipindi kigumu lakini kupitia mwelekeo huo wameshatoa ajira kwa wapagazji 20,000 ambao kipato chao kilitokomea na matetemeko hayo ya mwezi Aprili na Mei mwaka huu.

Bwana Ragan amesema kwa miezi miwili iliyopita wameshapatia msaada wa vyakula watu Milioni Mbili kwenye maeneo ya milimani yaliyo vigumu zaidi kufikika.

Hata hivyo amesema kuelekea mkutano wa wahisani wa kimataifa kwa Nepal, WFP inaonya kuwa ukata unakaribia kuikumba kwa kuwa ombi lake la kufadhili operesheni za Nepal  limechangiwa kwa asilimia 38 tu hadi sasa wakati huu ambapo dola Milioni 74 zahitajika kwa ajili ya usaidizi hadi mwishoni mwa mwaka