Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO na UNODC zataka hatua zichukuliwe kuzuia unyanyasaji na ulaghai katika kutoa ajira

ILO na UNODC zataka hatua zichukuliwe kuzuia unyanyasaji na ulaghai katika kutoa ajira

Shirika la Kazi Duniani, ILO na Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu dawa na uhalifu, UNODC, yameungana kupigia chepuo mifumo bora ya kuwapa watu ajira ndani ya nchi na kimataifa, ili kukabiliana na mienendo ya ulaghai katika utoaji ajira. Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Mashirika ya ILO na UNODC yametoa wito kwa serikali, wadau wa kijamii, wafanyabiashara na mashirika mengine ya kimataifa kuimarisha juhudi zao katika kukabiliana na mifumo ya utoaji ajira inayonyanyasa na yenye ulaghai.

Mashirika hayo yamesema, ingawa kuhama kwa wafanyakazi kuna manufaa kwa mamilioni ya wafanyakazi na familia zao, kwa wengi, kuna gharama na madhara makubwa, hususan pale isipodhibitiwa vyema.

Kumekuwa na shaka kote duniani kuhusu mashirika laghai ya ajira na wasafirishaji haramu ambao huwanyanyasa wafanyakazi wasio na stadi za kutosha na wahamiaji, kwa kuwadanganya kuhusu aina ya kazi wanayokwenda kufanya, kuwanyang’anya paspoti zao, kukata mishahara yao, kutosa ada ya usajili kwa ajira na kuwaweka utumwa na vitisho vya ukatili na kufukuzwa.

ILO imeanzisha mkakati wa utoaji ajira wenye haki, ambao unalenga kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu na ajira za kulazimishwa ndani ya nchi na kimataifa, pamoja na kuwalinda wafanyakazi wahamiaji kutokana na mikakati ya utoaji ajira yenye ulaghai.